Treni ya abiria iliyokuwa inatoka Dar Es Salaam kuelekea Bara (Mwanza, Mpanda na Kigoma kupitia Tabora) imepata ajali Wilayani Bahi umbali wa KM 40 kutoka Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema:
“Treni ilikuwa na Watu zaidi ya 700, kuna mvua zinanyesha sana, bado hatujajua chanzo cha ajali ila kichwa kimeanguka, taarifa za awali zinaonesha Mfanyakazi wetu mmoja amefariki na abiria wawili wamefariki, nilikuwa likizo nimeikatisha naelekea eneo la tukio,” amesema Kadogosa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Best Magoma amethibitisha kupokea majeruhi 61 ambao kati yao 41 ni wanaume na 19 ni wa kike.
“Kimsingi wengi wao wana hali nzuri, wenye hali zisizo nzuri sana ni watatu, wengi wamevunjika na mmoja wao yupo theatre akiendelea na matibabu” amesema Dkt. Magoma.
“Tuliowalaza mpaka sasa ni wagonjwa 21 wengine tuliweza kuwahudumia wakaonekana wako stable wakaruhusiwa kwenda nyumbani” ameeleza Dkt. Magoma.