Klabu ya Newcastle imethibitisha kumsajili Kieran Trippier kutoka klabu ya Atlético Madrid kwa ada ya Pauni Milioni 12.
Beki huyo wa pembeni mwenye umri wa miaka 31 amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa chini ya kocha mkuu wa klabu Eddie Howe.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Trippier amesema “Nimefurahi kujiunga na klabu hii nzuri. Nilifurahia sana wakati wangu huko Madrid, lakini nilipofahamu kupendezwa na Newcastle United, na baada ya kufanya kazi na Eddie Howe hapo awali, nilijua hapa ndipo nilitaka kuwa”
“Ninafahamu kuna changamoto nyingi mbele yetu lakini najua mahitaji ya Ligi Kuu (EPL) vizuri na najua hii ni klabu yenye wachezaji wenye vipaji na wazuri”.
Kwa upande wake Kocha mkuu wa Newcastle United Eddie Howe amesema “Nimefurahi sana kumkaribisha Kieran Newcastle United. Kwa muda mrefu nimevutiwa na uwezo wake.
“Ningependa kuwashukuru wote waliohusika, hasa wamiliki wetu”
Trippier alianza kucheza soka katika klabu ya karibu ya Manchester City na akaingia kwenye soka la wakubwa kwa mkopo katika klabu ya Barnsley na Burnley kipindi hiko kocha alikuwa Eddie Howe ambaye sasa ndio kocha wa Newcastle.