Rais wa Marekani, Donald Trump ameagiza nyaraka 2,800 za matokeo ya upelelezi wa mauaji ya Rais wa 35 wa nchi hiyo, John F Kennedy maarufu kama JFK, ziwekwe wazi.

Awali, kulikuwa na mengi yasiyo na uthibitisho ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi kutuhumiwa kuhusika kusuka njama za mauaji ya JFK yaliyofanyika Dallas mwaka 1963.

Mwaka 1992, Bunge la Congress liliweka sheria iliyoagiza nyaraka hizo zenye kurasa milioni tano kuwekwa wazi ndani ya kipindi cha miaka 25. Hivyo, siku ya mwisho ilikuwa jana (Alhamisi).

Trump alieleza kuwa wananchi wa Marekani wana haki ya kuelezwa ukweli kuhusu mauaji ya aliyekuwa Rais wao. Trump aliandika, “Kwahiyo, nina amuru leo kuwa nyaraka hizo ziwekwe wazi.”

Hata hivyo, Rais Trump alisema kuwa baadhi ya nyaraka zitaendelea kuwa siri ya vyombo vya usalama kutokana na kubeba mambo yanayohusu usalama wa taifa hilo.

Rais Kennedy aliuawa kwa kupigwa risasi Novemba 22, 1963 alipokuwa akisafiri ndani ya gari la wazi huko Dallas.

Gavana wa jimbo la Texas, John Connally aliyekuwa amekaa mbele ya Rais Kennedy alijeruhiwa. Pia, afisa wa jeshi la polisi, JD Tippit aliuawa muda mfupi baadae.

Serikali ilimkamata Lee Harvey Oswald kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Rais Kennedy na Tippit, lakini alikana tuhuma hizo akidai kuwa yeye alitumika tu kama ‘mbuzi wa kafara.’

Novemba 24, Oswald aliuawa pia kwa kupigwa risasi akiwa Dallas, katika eneo linalomilikiwa na jeshi la polisi. Aliyemuua ni Jack Ruby, mmiliki wa bar moja eneo hilo.

Sugu apinga adhabu ya kufungiwa vyombo vya habari
Barrick yaweka sharti la kusafirisha makinikia kulipa Sh bilioni 700