Bundi la kuchunguzwa limeendelea kutua juu ya paa la Ikulu ya Marekani, ambapo mkuu wa nchi hiyo, Rais Donald Trump anakabiliwa na uchunguzi mwingine kwa tuhuma za kuzuia sheria isitekelezwe.

Gazeti la Washington Post limeeleza kuwa Trump anachunguzwa na jopo la wanasheria likiongozwa na mwanasheria maalum Robert Mueller, taarifa ambazo zilitolewa kwa gazeti hilo na maafisa wa FBI.

Muller pia anaongoza uchunguzi wa FBI kubaini kama Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani uliomuingiza madarakani Rais Trump, lakini pia unalenga kubaini endapo Trump alihusika katika suala hilo.

Wanasheria wa Trump wamelaani kitendo cha FBI kutoa taarifa hizo kwenye gazeti hilo, hatua ambayo gazeti hilo limedai kuwa ni hatua kubwa kwa uchunguzi ulioanzishwa.

Rais Trump anahusishwa na kuwa na uhusiano wa karibu na Urusi, ambapo ushirikiano kati ya nchi hizo zenye historia ya uhasimu ilikuwa moja kati ya ahadi zake wakati wa kampeni. Trump alieleza kuwa ili kukabiliana na kundi la kigaidi linalojiita Islamic States of Iraq and Syria (ISIS), ni muhimu nchi hizo kushirikiana.

Kwa mujibu wa Washington Post, maafisa wa FBI wamesema kuwa uchunguzi dhidi ya Trump juu ya suala hilo ulianza mapema baada ya kumfukuza kazi mkuu wa FBI, James Comey mwezi Mei mwaka huu.

 

Trump alidaiwa kumshawishi Comey kutoendelea na uchunguzi dhidi ya mshauri wake wa masuala ya usalama, Michael Flynn aliyekuwa akidaiwa kuwa na uhusiano wenye utata na balozi wa Urusi.

Idadi ya vifo yaongezeka jengo lililoteketea kwa moto Uingereza
?Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Juni 15, 2017