Mshauri mkuu wa Rais wa Marekani Donald Trump, John Bolton amesema kuwa rais wa nchi hiyo yuko tayari kufanya mazungumzo kwa mara ya tatu na rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ambapo amesema kuwa ni Jukumu la Korea Kaskazini kuamua.
Bolton amesema kuwa Marekani kwa upande wake iko tayari kufanya mazungumzo hayo hivyo ni jukumu la Korea Kaskazini kuamua ni wapi mkutano huo ufanyike.
Kauli yake imetolewa kwenye mkesha wa kutimia mwaka mmoja tangu mkutano wa kihistoria baina ya Trump na Kim ambao ulifanyika Singapore.
Aidha, mapema hii leo, Korea Kaskazini imeitaka Marekani kuachana na sera ya uhasama, ikisema haiwezi kufanya kazi na kile ilichokiita, ”kiburi na maamuzi ya upande mmoja”.
Hata hivyo, katika mkutano wa Singapore, viongozi hao wawili walisaini makubaliano ya kuelekea kuondoa kabisa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea, lakini mkutano wa pili nchini Vietnam uliambulia patupu, baada ya kushindwa kuelewana juu ya hatua ambazo Korea Kaskazini ilipaswa kuzichukua ili kuondolewa sehemu ya vikwazo ilivyowekewa.