Rais wa Marekani Donald Trump amewataka wamarekani kuwa wamoja katika kulinda maslahi ya nchi hiyo ambayo inatajwa kuwa imegawanyika katika maeneo mengi huku mifumo kadhaa ukiwemo wa uhamiaji ukiwa katika hali mbaya.
Rais Trump ametumia nafasi hiyo mbele ya Bunge la Congress ambalo kuzungumzia masuala muhimu ya Taifa na hata kurejelea yale ambayo yanapigiwa kelele duniani kote.
“Marekani ni Taifa lenye huruma na uungwana. Tunaona fahari kuwa tunafanya zaidi ya taifa lolote mahali popote duniani katika kusaidia wahitaji, wanaohangaika na walioko katika haki ngumu duniani kote. Lalini kama Rais wa Marekani ninao wajibu wa kuonesha uungwana na huruma hiyo kwa watoto wa Marekani, wafanyakazi wa Marekani wanaohangaika na jamii za Marekani zilizosahaulika.
“Nahitaji vijana wetu wakue na kufanikiwa katika mambo makubwa. Nataka watu wetu maskini wapate fursa ya kukua. Kwa hiyo usiku huu nakaribisha pande zote ili tufanye kazi, Democrats na Republican, kuwalinda raia wetu wa mazingira tofauti, rangi dini na imani.
“Wajibu wangu na wajibu mtakatifu wa kila kiongozi aliyechaguliwa ndani ya jengo hili ni kuwalinda wamarekani kulinda usalama wao, familia zao, jamii zao na haki yao katika ndoto ya Marekani kwa sababu wamarekani wanazo ndoto pia.”
Rais Trump amezungumzia pia mpango wa kuwadhibiti ipasavyo wahamiaji wanaodaiwa kusababisha matatizo mengi ndani ya Marekani ikiwemo uhalifu. Moja ya njia za kudhibiti hali hiyo ni kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico. Hata hivyo Democtats wanaiona mipango mingi ya Trump kama ya msimamo mkali na hivyo kuwepo uwezekano wa kutomuunga mkono itakapopelekwa kwenye Bunge la Congress kwa uamuzi wa mwisho.
Kama hiyo haitoshi, Rais Trump akatonesha donda la kuutambua mji wa Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel.
“Mwezi uliopita nilichukua hatua ambayo iliungwa mkono kwa kauli moja na seneti miezi kadhaa ya awali: Nilitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. (Makofi) Muda mfupi baada ya hapo, makumi ya nchi yalipiga kura ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa mataifa dhidi ya Mamlaka ya Dola Huru ya Marekani kufanya uamuzi huu. Kwa mwaka 2016, walipa kodi wa Marekani walipeleka kwa uaminifu kabisa katika nchi hizo zaidi ya dola za Marekani bilioni 20 za msaada hali ndiyo hiyo, usiku huu ninaliomba Bunge la Congress kupitisha sheria ya kusaidia kuhakikisha dola za misaada ya Marekani ya nje mara zote ina nufaisha maslahi ya Marekani, na iende tu kwa marafiki wa Marekani na siyo maadui wa Marekani.” Alimalizia Trump na kushangiliwa kwa nguvu na wajumbe.