Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kufuta mpango wa kufanya mazungumzo na Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani na viongozi waandamizi wa kundi la Taliban yaliyolenga kutafuta amani nchini humo.

Trump ametangaza uamuzi wake kupitia mtandao wa Twitter, akieleza kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kundi la Taliban kukiri hadharani kuwa lilitekeleza shambulizi lililosababisha kifo cha askari wa jeshi la Marekani jijini Kabul.

Muongoza mazungumzo ya mpango huo wa amani kutoka Marekani, Zalmay Khalilzad alikuwa ametangaza kuwepo kwa mkutano wa pamoja wa makubaliano kati ya pande hizo mbili, Jumatatu wiki ijayo.

Mpango wa Trump kukutana na viongozi hao wa Afghanistan na Taliban ulitokana na mazungumzo ya mara kadhaa yaliyofanywa kati ya Marekani na wawakilishi wa kundi la Taliban yaliyofanyika jijini Doha, Qatar.

“Kwa bahati mbaya, ili kujenga ushawishi wa uongo, kundi la Taliban limekiri kufanya shambulizi ambalo limemuua mmoja kati ya wanajeshi wetu wakuu sana. Kwahiyo, nimefuta mara moja mkutano na ninasitisha mazungumzo ya kutafuta amani,” Rais Trump ametweet.

Katika mazungumzo ya awali, walikuwa wamekubaliana kuwa Marekani itawarudisha nyumbani zaidi ya wanajeshi 5,400 kutoka Afghanistan ndani ya kipindi cha wiki 20. Hadi sasa kuna vikosi vya wanajeshi 14,000 vya Marekani ndani ya Afghanistan.

Marekani inaunga mkono Serikali ya Afghanistan inayopambana vikali na kundi la Taliban ambalo liliwahi kuiongoza nchi hiyo baada ya kufanya mapinduzi.

Taliban iliingia kwenye mgororo na Marekani baada ya kumtunza Osama Bin Laden ikiwa chini ya uongozi wa Mullah Omar.

Hakimu akamatwa kwa wizi wa madawa ya kulevya, alimfunga mtuhumiwa miaka 30
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 8, 2019