Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza hali ya dharura inayolenga kulinda mitandao ya mawasilinao ya taifa hilo.

Trump ametia sahihi amri ya rais inayopiga marufuku ununuzi ama matumizi ya vifaa kutoka kwa kampuni ambazo zinatishia usalama wa taifa hilo na usalama wa raia wa Marekani.

Afisa mmoja kutoka Ikulu ya Marekani amesema kuwa hakuna nchi wala kampuni maalum zilizolengwa na amri hiyo, huku msemaji wa Ikulu, Sarah Sanders akisema serikali ya Trump itafanya iwezavyo kuifanya Marekani salama na vile vile kuilinda dhidi ya maadui wakigeni.

Aidha, amri hiyo imeipa nguvu wizara ya biashara ya Marekani kuzuia kampuni za kimarekani kufanya biashara na kampuni kadhaa za kigeni, japo tangazo hilo halijaitaja moja kwa moja kampuni ya Huawei ambayo ni kampuni kubwa katika kutoa huduma za mtandao wa kasi zaidi wa 5G lakini amri hiyo inatafsiriwa kwamba imeilenga kampuni hiyo.

Hayo yanajiri wakati Marekani na China ziko katika mvutanao wa kibiashara, hivyo basi imeonekana kwamba Marekani imechukua uamuzi huo kutokana na wasiwasi wake mkubwa wa kuwa kampuni ya Huawei inatumika na serikali ya China kuipeleleza Marekani.

Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa na Kampuni ya Huawei imesema kuwa iko tayari kuzungumza na serikali ya Marekani na kukubaliana kubuni mbinu bora zitakazo wahakikishia usalama wa bidhaa zake.

 

Video: Fahamu utamaduni wa kumkata kidole mwanamke aliyefiwa
Serikali haijasema mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni hatari- Dkt. Abbas