Rais wa Marekani, Donald Trump ameanza kuzifanyia kazi ahadi zake baada ya kusaini amri ya kuzuia kwa muda wakimbizi kutoka Syria na nchi nyingine zinazoongozwa kwa sharia, kuingia nchini humo hadi hapo atakapotangaza tena kuruhusu.
Syria inatajwa kuwa sehemu ya ngome ya kundi la kigaidi linalojiita Islamic State of Iraq and Syria, linaloilenga pia Marekani na nchi nyingine za Magharibi.
Kwa mujibu wa CNN, Rais Trump amesaini amri hiyo katika kile alichokiita ‘mkakati wa kuzuia magaidi kuingia Marekani’. Kupitia mkakati huo ameeleza kuwa watu wote watakaotaka kuingia nchini Marekani kutoka nchi zinazofahamika kuwa na ugaidi au kufuata msimamo mkali wa kidini watafanyiwa ukaguzi wa hali ya juu kabla ya kupata kibali.
Aidha, Trump pia amesaini amri nyingine itakayosababisha wakimbizi kutoka nchi zote duniani kukataliwa kuingia Marekani kwa kipindi cha miezi mine.
Wageni wanaotaka kutembelea Marekani kutoka nchi sita zinazotambulika kama nchi zinazoendeshwa kwa kufuata sharia wamezuiwa kuingia Marekani kwa kipindi cha miezi mitatu.
Akizungumza katika sherehe za kumuapisha Generali James Mattis, Trump alisema, “nimeanzisha hatua za ukaguzi mpya kuhakikisha naondoa makundi yenye itikadi kali za kigaidi kutoingia Marekani. Tunataka kuwaruhusu wale tu ambao wataingia nchini kwetu kuipenda nchi yetu na watu wake.”
Uamuzi huo wa Trump umelaaniwa na kupingwa vikali na makundi mbalimbali ya Haki za Binadamu. Amri hiyo imechukuliwa kuwa ya kibaguzi kwani amewapa nafasi ya upendele wakimbizi ambao sio wa imani ya Kiislamu kuingia nchini humo.