Rais wa Marekani, Donald Trump amekumbana na maandamano makubwa nchini Ubelgiji mara baada ya kuwasili akitokea nchini Italy katika ziara ya kutembelea nchi sita zilizoko katika orodha.
Maandamano hayo yamefanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Brussels kumpinga Trump kufanya ziara na kuhudhuria katika mkutano wa viongozi wa ulaya na umoja wa kujihami barani ulaya NATO.
Waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yaliandikwa, “hatumtaki Trump” wamedai kuwa wamefanya maandamano hayo ya kumpinga Rais Trump kufuatia matamshi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini Marekani pale aliposema mji mkuu wa Ubelgiji yaani Brussels kuwa ni sawa na Jehanam.
Hata hivyo, Trump amekutana na mwenyeji wake mfalme Philipe na Malkia Mathlide na kufanya mazungumzo kabla ya kuanza mkutano na viongozi wa ulaya ambapo wanatarajia kuzungumzia masuala ya usalama na kuimarisha uhusiano.
.Trump amewasili nchini Ubelgiji akitokea Rome nchini Italy ambako alikutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis na baadhi ya viongozi wakuu wa nchi hiyo.