Rais wa Marekani, Donald Trump amewasimulia wananchi wake jinsi alivyowashuhudia raia wa Korea Kusini wakitokwa machozi ya furaha baada ya kumuona anakanyaga ardhi ya jirani zao waliokuwa mahasimu, Korea Kaskazini.
Jana, Rais huyo wa Marekani aliandika historia ya kipekee alipokutana na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un kwenye mpaka wa Korea Kusini na Kaskazini (DZN).
Baada ya kushikana mkono na Kim, Trump aliitikia wito wa kiongozi huyo na kuingia kwenye ardhi ya Korea Kaskazini akiandika historia ya kuwa Rais wa kwanza wa Marekani aliyeko madarakani kufanya hivyo.
“Nilifurahi na ilikuwa heshima kukutana na Mwenyekiti Kim pale mpakani, nilifika kwa mara ya kwanza DZM na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in alisema tulifanya jambo la kihistoria na mimi naamini hivyo,” alisema Trump.
“Mwenyekiti Kim alinialika niingie kwenye ardhi ya Korea Kaskazini, nilimwambia ni heshima kwangu kufanya hivyo na niliingia tukashikana mkono wote, niliwaona raia wa Korea Kusini wakitokwa na machozi ya furaha kuona hilo,” aliongeza.
Raia wa Korea Kusini waliokuwa kwenye eneo hilo ambalo liliwakutanisha marais watatu walifurahi kuona uhasama kati ya mataifa hayo unaendelea kuvunjwa na moshi mweupe wa amani unaanza kutanda.
Rais Trump alimualika Kim kupitia akaunti yake ya Twitter, alipoeleza kuwa kama anaiona tweet yake anapenda kukutana naye atakapokuwa mpakani na amsalimie ‘hello’.
“Ule mtandao wa kijamii ni jitu kubwa sana, lilifanya mambo yote yakawezekana na mimi nafurahi kuona Mwenyekiti Kim aliitikia wito ule, mwisho tulifanya mkutano mkubwa na wenye matunda zaidi tukiwa na Rais Moon pia,” alisema Trump.
Huo ulikuwa mkutano wa tatu ambao wengi hawakuutarajia kati ya Trump na Kim, ikiwa mkutano wa kwanza ulifanyika Singapole na wa pili ambao ulivunjika ulifanyika Vietnam.