Rais wa Marekani, Donald Trump amewavaa wabunge wa chama cha Democratic walioapa kuhakikisha wanapata wito wa kisheria wa nyaraka muhimu za mawasiliano ya Ikulu wiki hii, wakitaka kumuondoa madarakani kwa matumizi mabaya ya ofisi.

Wabunge hao wanataka kupata nyaraka muhimu kuhusu mawasiliano kati ya Rais Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky wakidai kuwa nyaraka hizo zitaanika ukweli kuhusu tuhuma za mawasiliano hayo kutaka kumuumiza mpinzani wake, Joe Biden kwa sababu binafsi.

Rais Trump amepinga vikali hatua za wawakilishi hao wa Democratic akieleza kuwa wamekosa uaminifu na wanachopanga ni kubariki uhaini.

Hatua za kutaka kumng’oa madarakani Trump zimetokana na taarifa zilizotolewa na ‘mtoa taarifa’ akilalamika kuhusu mazungumzo ya Julai 25, 2019 kati ya Trump na Zelensky.

Wajumbe wa Democratic wanadai kuwa baada ya mazungumzo hayo, Trump alichukua uamuzi wa kusitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Hivyo, wanadai inaweza kuwa ni shinikizo la kutaka Rais Zelensky afanye uchunguzi dhidi ya Biden na mwanaye wa kiume.

Wamedai kuna dalili kuwa uamuzi huo ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha Katiba ya Taifa hilo, akiwa na lengo la kufifisha upinzani wa Biden dhidi yake katika uchaguzi wa urais wa 2020.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa babari kati yake na Rais wa Finland, Sauli Niinistö, Trump alieleza kuwa mtu anayeitwa ‘mtoa taarifa’ kwenye sakata hilo kuwa anapaswa kuangaliwa kama mpelelezi na kwamba Mwenyekiti wa Kamati ya Intelijensia cha Ikulu, Adam Schiff anapaswa kujiuzulu.

“Hii nchi inapaswa kumtafuta namna ya kumfahamu huyu mtu ni nani. Kwakweli, huyu mtu anapaswa naye kuangaliwa kama mtu anayetaka kufanya uhaini,” alisema Trump na kuongeza kuwa anaamini ndiye aliyemsaidia huyo anayeitwa ‘mtoa taarifa’kuandika malalamiko yake lakini akashindwa kutoa udhibitisho.

Rais Trump ameendelea kusisitiza kuwa tuhuma hizo ni za kihuni na za kizushi huku akiendelea kuahidi kushirikiana na wawakilishi wabunge wote.

Mratibu mkuu wa vikwazo Marekani kujiuzulu
Roy Keane aziponda Manchester United, Arsenal