Wagombea wakuu wa urais nchini Marekani, Donald Trump wa Republican na Joe Biden wa Democratic, wamejitokeza katika vituo viwili tofauti vya televisheni, kila mmoja akimtuhumu mwenzake juu ya namna anavyouchukulia ugonjwa wa COVID-19.
Katika kile kinachoonekana kama mdahalo baina yao, vituo viwili hasimu vya NBC na ABC nchini Marekani viliwaalika wagombea hao mahasimu kwa mahojiano ambayo yalirushwa moja kwa moja na kwa wakati mmoja Oktoba 15.
Rais Trump aliyehojiwa na kituo cha Runinga cha NBC mjini Miami alikataa kusema waziwazi endapo wakati wa mdahalo wake wa kwanza na Biden, alipimwa na kugundulika kutokuwa na virusi vya corona.
Trump aliugua ugonjwa huo siku chache baada ya mdahalo wa tarehe 29 Septemba, na kupelekea kulazwa hospitalini.
Kwa upande wake, Biden akihojiwa na kituo cha Runinga cha ABC, mjini Phila-delphia, amesema Trump hakuyachukulia maradhi ya Covid 19 kwa umakini na zaidi ya wamarekani 210,000 wamefariki kutokana na janga hilo.
Aidha kwa wengi, mahojiano hayo yamechukuliwa kama sehemu ya pili ya mdahalo wa uso kwa macho kati ya Trump na Biden, ambapo awali ulikuwa umepangwa kufanyika Oktoba 15 lakini Trump akajitoa baada ya waandaaji kuamua ufanyike kupitia mtandao baada ya Trump kuugua COVID-19 wiki mbili zilizopita.