Rais wa Marekani, Donald Trump ameionya Korea Kaskazini huku akiahidi kuwa iwapo nchi hiyo itaendelea na vitendo vyake vya uchokozi basi itakabiliwa na hatua kali ambazo dunia haijawahi kuzishuhudia
Trump ametoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Bedminster New Jersey ambako yuko mapumzikoni, amesema kama Korea Kaskazini itaendelea na mpango wake basi dunia itashangaa.
Aidha, Trump hakutoa maelezo zaidi kuhusu hatua zitakazochukuliwa na Marekani huku vita ya maneno ikizidi kuchukua nafasi kubwa kati ya nchi hizo kwa kila mmoja akitoa onyo kwa mwenzie.
Marekani katika siku za hivi karibuni imekuwa ikifanya juhudi za kuongeza mbinyo kwa Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na kushawishi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini dhidi ya mpango wake wa majaribio ya silaha za nyuklia.
Katika ukurasa wake wa twitter, Rais Donald Trump amesema kuwa “baada ya kushindwa miaka mingi hatimaye sasa mataifa yanaungana pamoja ili kutafuta njia ya kukabiliana na hatari inayoweza kusababishwa na Korea Kaskazini tunapaswa kuwa thabiti”
Hata hivyo, siku za hivi karibuni Korea Kaskazini ilisema haina mpango wa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya yeyote isipokuwa Marekani na kuongeza kuwa katika mazingira yoyote haitakuwa tayari kujadili juu ya mpango wake unaohusiana na silaha hizo.