Rais wa Marekani, Donald Trump ameahidi kufuta sheria inayowapa haki ya uraia watu wote wanaozaliwa ndani ya mipaka ya taifa hilo lenye nguvu duniani.
Trump ametoa kauli hiyo wiki hii wakati harakati za kampeni za uchaguzi wa magavana nchini humo zikiwa zimeshika kasi.
“Sisi ndilo taifa pekee duniani ambalo mtu [raia wa kigeni] anakuja hapa anazaa mtoto halafu huyo mtoto anakua raia wa Marekani. Huu ni upuuzi na unatakiwa kukoma,” alisema Trump.
Hata hivyo, tofauti na kauli yake, mbali na Marekani mataifa mengine yanayotoa uraia kwa kila anayezaliwa nchini humo ni pamoja na Canada na Mexico
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameonesha shaka ya namna Trump atakavyopata baraka za Bunge la Congress kuhusu mpango huo.
Katika hatua nyingine, Rais Trump ameendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa kwenye kampeni zake, ikiwa imebaki wiki moja tu taifa hilo liwachague magavana wa majimbo 36 kati ya 50, baada ya msanii Pharrell Williams kuandika barua ya kumzuia kutumia wimbo wake wa ‘Happy’ kwenye mikutano yake ya kampeni.
Hatua hiyo ya Pharrell, inafanana na hatua zilizowahi kuchukuliwa na The Rolling Stones mwaka 2016, ambapo walimzuia Trump kutotumia wimbo wao ‘You Can’t Always Get What You Want’.
Lakini pia, mwanzoni mwa mwezi huu, familia na timu ya marehemu Prince ilimzuia kutumia wimbo wa Purple Rain.
Hata hivyo, Trump anaungwa mkono pia na wasanii kadhaa wakubwa kama Kanye West na Kid Rock; na hivyo anaweza kutumia nyimbo zao bila tatizo.
Rais Trump ametamba kuwa chama chake cha Republican kitashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Novemba 6, akieleza kuwa ushindi huo utatokana na uimara wa utawala wake.