Rais wa Marekani, Donald Trump anatarajia kufanya mazungumzo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Marekani (White House) mwezi huu.
Taarifa iliyotolewa na idara ya mawasiliano ya White House imeeleza kuwa Kenyatta atafika katika ikulu hiyo Agosti 27 mwaka huu, na kwamba moja kati ya mambo watakayojadili viongozi hao ni uhusiano wa nchi hizo mbili.
Kadhalika, taarifa hiyo imeeleza kuwa Trump na Kenyatta watazungumzia hali ya usalama katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki.
“Kenya ni washirika muhimu wa Marekani na Rais Trump anatarajia kujadiliana na Rais wa Kenya ili kuimarisha na kutanua ushirika wa kimkakati kwa kuzingatia misingi ya demokrasia,” imeeleza taarifa hiyo ya White House.
Aliongeza kuwa amani na utulivu wa bara la Afrika ni sehemu ya mjadala muhimu wa wakuu hao wa nchi watakapokutana mwishoni mwa mwezi huu.
Marekani na Kenya wanashirikiana pamoja na vikosi vya Umoja wa Afrika kupambana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia.
Kenyatta anaweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza Afrika Mashariki kuzulu Ikulu ya Marekani lakini pia Rais wa tatu barani Afrika akiwafuatia Marais wa Misri na wa Nigeria.