Baada ya kutofautiana kimawazo na kufikia hatau ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurungenzi Simba SC kususia vikao, imeripotiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Salim Abdallah ‘Try Again’ amemaliza tofauti zilizokuwa zikiwatafuna ndani kwa ndani.
Kassim Dewji ambaye alitangazwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili baada ya kufariki kwa Zacharia Hanspope, alikua wa kwanza kutoka hadharani na kutangaza tofauti zilizopo kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC.
Taarifa iliyopatikana leo jumatano jioni (Juni 29) imeeleza kuwa, Mwenyekiti Salim Abdallah ‘Try Again’ aliwaita baadhi ya wajumbe ambao walioneshwa kutokua tayari kuendelea na vikao vya bodi na kuzungumza nao, hadi kumaliza tofauti zilizokuwepo.
Taarfa hizo huenda zikawa kheri kwa Simba SC, ambayo kwa sasa inajipanga na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa.
Simba SC imemaliza msimu wa 2021/22 bila kuwa na taji la ubingwa wa Tanzania Bara, ikiambulia ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka kidedea kisiwani Unguja kwenye michuano hiyo, ambayo hushirikisha timu za Zanzibar na Tanzania Bara kwa ajili ya Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964.