Mwenyekiyi wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amekanusha uvumi wa klabu hiyo kuwa mbioni kumsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka Burundi Saido Ntibazonkiza.
Saido ameachana na Young Africans baada ya kumaliza mkataba wake mwishoni mwa mwezi Mei, huku akihusishwa na utovu wa nidhamu kwa kutoroka kambini wakati timu ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Simba SC.
Try Again amesema: ”Saido Ntibazonkiza ni mchezaji mzuri hata mimi ninampenda lakini kama timu lazima tulinde misingi ya nidhamu. Nimesikia ameachwa Young Africans kwa sababu ya utovu wa nidhamu.”
“Sisi Simba SC Tanzania tukisajili mchezaji ambaye timu nyingine imemuacha kwa sababu ya matatizo ya kinidhamu maana yake tutakuwa hatuheshimu kile kilichofanywa na viongozi wenzetu kwingine. Tunaweza kusajili mchezaji kwa kuvunja mkataba wake au kama yuko huru lakini sio aliyeachwa kwa sababu za kinidhamu.”
Simba SC imeshaweka wazi mpango wa kukifumua kikosi chake kuelekea msimu wa usajili, huku ikiahidi kusajili wachezaji wenye kiu ya mafanikio ‘Mataji’ ambao wataungana na watakaosalia kikosini.
Msimu huu Simba SC imepoteza mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ huku ikifika Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.