Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Klabu ya Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ amevunja ukimya na kuliweka wazi suala la Kiungo Mshambuliaji Hassan Dilinga anayetajwa kuwachwa kwenye usajili wa klabu hiyo.
Dilunga hakuwa sehemu ya Wachezaji waliotambulishwa wakati wa Tamasha la Simba ‘Simba Day’ mnamo Agosti 08 mwaka huu, na baadae kuibua hoja mbalimbali kutoka kwa Mashabiki ambao walihoji kuachwa kwa kiungo huyo.
‘Try Again’ amesema Kiungo huyo aliyefanyiwa upasuaji msimu uliopita huko Afrika Kusini bado anaendelea kuwa chini ya ungalizi wa Klabu ya Simba SC, katika kipindi hiki ambacho bado anajiuguza.
Amesema endapo Dilunga atapona majeraha yake huenda akarejeshwa kwenye kikosi cha Simba SC kupitia Dirisha Dogo la Usajili, hivyo amewataka Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuwa watulivu na kupuuza taarifa za mitandaoni.
“Dilunga aliumia akiwa katika majukumu yake ndani ya klabu ya Simba SC, baada ya kumpeleka Afrika Kusini kutibiwa sasa hivi yuko chini ya uangalizi wa madaktari wa Simba SC.
“Sisi tutaendelea naye mpaka Dirisha Dogo tuone hali yake, kama atakuwa amepona bado tunamuhitaji sana. Naamini Mungu atamsaidia atarejea katika hali yake, kwani bado mchango wake tunauthamini,” amesema Try Again.