Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeahidi kuandaa mikakati madhubuti kuhakikisha timu yao inaifunga Power Dynamos katika mhezo wa marudiano na kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mhezo wa Mkondo wa Kwanza, Simba SC ikiwa ugenini ililazimisha sare ya mabao 2-2 hivyo ili kutinga hatua ya makundi inahitaji suluhu, sare ya bao 1-1 au ushindi wowote wa mabao katika mechi ya marudiano itakayochezwa Dar es Salaam Oktoba Mosi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema hawapo tayari kuona wanaondoshwa kwenye michuano hiyo, ndio maana watakuwa karibu na benchi lao la ufundi kufanikisha dhamira hiyo.
“Shabaha yetu kubwa ni kucheza hatua ya makundi na kufika angalau nusu fainali, tunajua siyo rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wetu, lakini sisi kama viongozi tutaongeza nguvu zetu kwa benchi la ufundi kwa kuandaa mikakati madhubuti itakayotusaidia kutimiza malengo yetu,” amesema Try Again.
Amesema hawapo tayari kurudia makosa ya miaka miwili iliyopita ambapo waliondoshwa raundi ya awali ya michuano hiyo na Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Kikosi cha Simba SC kilitarajiwa kurejea nchini jana Jumatatu (Septemba 18) majira ya jioni kikitokea Zambia na kitaingia kambiri moja kwa moja kujiandaa na mhezo wa raundi ya tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ya Tanga keshokutwa.