Uongozi Simba SC umeweka wazi licha ya kupata ushindi katika mchezo wao wa juzi Jumamosi (Oktoba 28) dhidi ya Ihefu FC, lakini mikakati mikubwa ni kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wao ujao dhidi ya Young Africans, huku wasisitiza kuwa Ihefu FC walikuwa ni sehemu ya maandalizi yao.
Simba SC iliendelea kupata ushindi katika mchezo wake wa sita juzi Jumamosi (Oktoba 28) kwa kuifunga Ihefu FC mabao 2-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa bado siku sita kabla Derby ya Kariakoo inayotarajiwa kuchezwa Novemba 5, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’, amesema kuwa japo wachezaji walikuwa na uchovu lakini waliweza kujituma na kupata ushindi.
“Ligi ni ngumu kila timu imejipanga, inakuja kivingine na kubadilika ni jambo jema kwa sababu inaonyesha ubora wa ligi yetu, hatukutarajia kuona Namungo FC anashinda dhidi ya Azam FC.
“Sisi Simba SC tunaenda kwa mipango hatutaki kukurupuka kila mechi tunaingia na mbinu zake tukishinda moja sawa, kikubwa na alama tatu. Hii mechi ya juzi imekuwa sehemu ya kujiandaa na Dabi dhidi ya watani wetu,” amesema Try Again.
Aliongeza kuwa Dabi ya Kariakoo ni mechi kubwa wanaiheshimu kwa kuwa itatoa ramani ya ubingwa. “Hatuwezi kuweka silaha zetu hadharani ila tumejpanga vizuri. Huwezi kusema kitu kuhusu ubingwa kwa mechi sita wakati kuna michezo 24 mbele, mapema sana licha ya nia yetu ni hiyo,” amesema Try Again