Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema Uongozi wa klabu hiyo unajua fika alama moja itawaingiza hatua ya Robo Fainali kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, lakini wanataka makubwa zaidi.
Simba SC itakuwa wenyeji wa mchezo huo Uwanja wa Benjamin Mkapa mapema mwezi ujao (April 03), huku ikihitaji alama moja tu! kufuzu hatua ya Robo Fainali ikitokea ‘Kundi A’ la michuano hiyo lenye timu nyingine kama Al Ahly ya Misri na Al Merrikh ya Sudan.
‘Try Again’ amesema lengo kubwa kuelekea mchezo dhidi ya AS Vita ni kuhakiksha kikosi chao kinaibuka na ushindi na kupata alama tatu, ambazo zitawahakikishia kubaki kwenye nafdasi ya kwanza ya ‘kundi A’.
“Tumebakiza pointi moja tu ili tuingie hatua ya robo fainali ila Simba hii haitaki kuwa na malengo madogo kama hayo tumekubaliana tupate alama zote tatu dhidi ya AS Vita,”
“Tukipata alama tatu ina maana tutakuwa tumefikisha pointi 13 ambazo hakuna timu itakayoweza kuzifikia katika kundi letu lakini hapo tutahitaji kuwa kinara wa kundi ili tuwe na wakati mzuri katika upangwaji wa ratiba ya robo fainali.
“Malengo yetu haya sio tu yapo kwa mdomo lakini yatatanguliwa na vitendo zaidi kwa sasa tupo kwenye msiba wa Hayati Magufuli na tunajipanga ili tujue aina ya maandalizi yetu yatakuwaje.”
“Watu wasidhani kama hatua hii tumefika kwa kubahatisha tulijipanga vyema kufikia mafanikio haya na bado tunataka kufika mbali zaidi msimu huu huu kama Mungu atatupa baraka zake zaidi.
“Simba ina nafasi kubwa kuingia hatua ya robo fainali lakini hayo sio malengo yetu makubwa,tunataka kuvuka hapo ikiwezekana kufika nusu na kama ratiba itakuwa nzuri kwetu tuko tayari hata kucheza fainali.
“Tumewaambia wachezaji na tunawaamini kwamba wanatakiwa kujiandaa kwa hatua ngumu zaidi, tuliunda timu kama hii kwa kutafuta malengo makubwa kama haya ambayo tunayo sasa kama klabu,” amesema ‘Try Again’.
Kwa upande wa AS Vita watahitaji kuutumia mchezo huo kama sehemu ya kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza, ambapo Simba waliibuka na ushindi wa 1-0, mjini Kinshasa, DR Congo.
Hata hivyo hii haitokua mara ya kwanza kwa AS Vita kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, kwani kamaitakumbukwa vyema timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge ilipoteza mbele ya Simba SC msimu wa 2018/19 kwa kufungwa 2-1, na kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi.
Mpaka sasa Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi A’ la michuano hiyo wakiwa wamejikusanyia alama 10, wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Al Ahly wenye alama 7, AS Vita wao wako kwenye nafasi ya tatu na alama 4, huku Al Merrikh ya Sudani wao wakiburuza mkia na alama 1.