Uongozi wa Klabu ya Simba SC, umesema kwa sasa unaendelea kujiweka sawa ili kuiwezesha timu yao inafanya vizuri katika Michuano ya CAF Super League, itakayoanza mwezi Oktoba 2023.
Simba SC itafungua Michuano hiyo dhidi ya timu itakayopangiwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Oktoba 20, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wanafanya mipango kuhakikisha timu yao inafanya vizuri bila ya kuangalia watakutana wapinzani wa aina gani katika michuano hiyo.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri, tulikuwa na wakati mzuri wa kujadili na maofisa wa CAF kuelekea maandalizi ya michuano hiyo,”amesema.
Amefafanua kuwa malengo yao ni kuona wanafika mbali kwa timu kuweza kupata matokeo mazuri katika kila mchezo bila ya kujali wanakutana na mpinzani wa aina gani.
Katika michuano hiyo ambayo itashirikisha timu nane Kundi la kwanza ikiwa na timu za Al Ahly ya Misri, Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Wydad Athelic (Morocco) na Esperance de Tunis (Tunisia).
Kundi la pili ni TP Mazembe (DR Congo), Petro Luanda (Angola) na Horoya Athletic Club (Guinea) na Simba SC ambao ni wenyeji wa michuano hiyo ambayo ni timú pekee kwa Afrika Mashariki kushiriki michuano hiyo.
Kauli ya kiongozi huyo, imekuja siku cháche baada ya Simba SC kuwapokea maofisa wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ ambao wapo nchini kwa ukaguzi wa maandalizi ya michuano hiyo.