Sakata la mkataba wa beki wa kushoto na nahodha msaidizi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ limeendelea kuchukua nafasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku kila mmoja akisema lake.

Mkataba wa ‘Tshabalala’ na Simba SC utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, huku taarifa zikieleza huenda akaikacha klabu hiyo na kujiunga na klabu nyingine ambayo itaonesha kuwa tayari kumlipa vizuri.

Hata hivyo mpaka sasa beki huyo anaendelea kuitumikia Simba SC kwa moyo wake wote, na mwishoni mwa juma lililopita alifunga bao muhimu dhidi ya Gwambina FC mjini Misungwi mkoani Mwanza, na kuipeleka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu hiyo iliyofikisha alama 58.

Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya Simba SC Haji Sunday Manara ni miongoni mwa wadau wanaotumia mitandao ya kijamii kuwasilisha maowazo yao kuhusu sakata la beki huyo.

Manara ameandika: “Zimbwe usije ukaiacha timu unayoishabikia,inayokuandaa kuwa lejendari,ukaenda utopoloni ,timu za hovyohovyo ambazo hazijui kesho yao,timu zisizoshinda mataji, kisa visumni vya kupita.”

“Barbra boss wangu wana Simba hawatotuelewa Zimbwe akitimkia utopolo,nakuomba ulimalize hili Ili watu wajue dhamira yetu.”

Afisa Mhamasishaji wa Young Africans Antonio Nugaz naye akajitosa katika sakata hilo, na ameonekana kama kumjibu Manara: “Muombee dua njema na acha afanye maamuzi yenye tabasamu endelevu.

Mjumbe wa kamati ya mashindano Young Africans na Mkurugenzi wa uwekezaji GSM Said Hersi naye akaandika:  “Msimu ujao tutazivunja benki zinazohifadhi watu.

Naye mchezaji wa zamani wa Young Africans ambaye kwa sasa ni mjumbe wa kamati ya ufundi klabuni hapo Seklojo Johnson Chambua naye ameandika: “Hakuna uzalendo kwenye pesa,kama kuna watu wanasaini kwa kwa milioni 250,300 hadi 700 na baadhi wanakaa benchi, mpeni Zimbwe hela msikimbilie kumnadi kwa ulejendari wala ushabiki.”

“Zimbwe maisha ya mpira ni ya nguvu kuisha na ni muda mfupi,amua kwa weledi.”

Pamoja na yote hayo kuandikwa kwenye mitandao ya kijamii, bado maamuzi ya mwisho yatakuwa kwa mchezaji mwenyewe (Mohamed Hussein ‘Tshabalala’) kusaini mkataba mpya na kuendelea kuitumikia Simba SC, ama kutafuta maisha mengine ya soka nje ya Mabingwa hao wa Tanzania Bara kwa misimu mitatu mfululizo.

Simba SC yaongoza kwa Tsh. 6.2 Bilioni (€2.20m)
Nugaz: Hatujakata tamaa ya ubingwa