Beki wa Kushoto na Nahodha Msaidizi wa Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amewatuliza Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Simba SC itaikaribisha Orlando Pirates jumapili (April 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, kuanzia saa moja usiku.

Tshabalala amesema Wachezaji wa Simba SC wapo tayari kuelekea mchezo huo na wanafahamu nini cha kufanya, ili kujiweka katika mazingira mazuri kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaounguruma Afrika Kusini Jumapili (April 24).

“Wapinzani wetu ni timu bora, ila naamini sisi ni bora pia na tumejipanga vizuri kupata matokeo chanya. Kila mchezaji anajua umuhimu wa mechi hii, tunacheza nyumbani hivyo tunahitaji ushindi ili kurahisisha kazi katika harakati zetu za kutinga nusu fainali na tupo tayari kupambana ili kufanikisha hilo,”

“Mashabiki zetu tunawakubali, wao ndio wanatupa nguvu kubwa ya kufanya vizuri uwanjani nawaomba wajitokeze kwa wingi kutusapoti na sisi hatutawaangusha.” amesema Tshabalala.

Simba SC ilitinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho, baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D kwa kufikisha alama 10, sawa na RS Berkane ya Morocco huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast na USGN zikitupwa nje.

Bigirimana atajwa kutua Young Africans 2022/23
Simba SC: Hatuna mpango wa kuomba TFF, TPLB