Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi wamekutana kwa mara ya kwanza nchini Kenya, tangu Kinshasa ilipoishutumu Kigali kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaofanya uharibifu mashariki mwa DRC.
Kukutana kwa viongozi hao wakuu wa nchi kunatokana na wito wa mkutano katika Ikulu ya Kenya wa Kongamano la tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuhusu mzozo wa DRC iliyoitishwa na Rais Uhuru Kenyatta, huku Rwanda ikiendelea kukanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23.
Marais wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Yoweri Museveni wa Uganda, Evariste Ndayishimiye wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini huku Tanzania ikiwakilishwa na Balozi wake nchini Kenya John Stephen Simbachawene.
Jumatano Juni 15, 2022, Rais Kenyatta alitoa wito wa kupelekwa kwa kikosi cha kanda ya EAC mashariki mwa DRC ili kurejesha amani, lakini Kinshasa ilisema haitakubali ushiriki wa Rwanda katika operesheni hiyo.
Wakuu wa jeshi la EAC walikutana Jumapili Juni 19, 2022, kabla ya mkutano huo wa Marais, kukamilisha maandalizi ya kupelekwa kwa kikosi cha pamoja katika eneo hilo lililoathiriwa na matukio ya uvunjifu wa amani.