Hatimae aliyekua nahodha na kiungo Young Africans Papy Kabamba Tshishimbi amekamilisha mpango wa kujiunga na klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Tshishimbi amekamilisha mpango huo, baada ya kumridhisha kocha Florent Ibenge ambaye aliamuru afanyiwe majaribio kwa majuma kadhaa, na sasa ataitumikia AS Vita kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kiungo huyo ambaye aliondoka Young Africans baada ya mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita, amesema ameamua kujiunga  na klabu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja kwa sababu hapendi kucheza soka katika ardhi ya nyumbani kwao.

“Ni kweli nimesaini AS Vita ya hapa nyumbani, wao walitaka nisaini mkataba wa miaka miwili, lakini mimi nimekataa, nimewaambia nataka nisaini mwaka mmoja. Unajua mimi sipendi sana kucheza soka huku kwetu, kwa sababu ukicheza soka nyumbani hata heshima inakuwa hakuna, unachukuliwa kama ni mchezaji wa kawaida tu, dharau inakuwa nyingi,” amesema Tshishimbi.

Kiungo huyo amesema alikamilisha taratibu za kusaini mkataba huo juma lililopita, na sasa anasubiri kibali cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka Tanzania ili aanze kuitumikia AS Vita.

Kiungo huyo alisajiliwa na Young Africans mwaka 2017, akitokea Mbabane Swallows ya nchini Swaziland (Eswatini).

Mourinho aipinga VAR hadharani
Cioaba atoa neno kabla hajawavaa Mtibwa Sugar