Nahodha na kiungo wa zamani wa Young Africans Papy Kabamba Tshishimbi, anakaribia kujiunga na klabu ya AS Vita ya nyumbano kwao Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo).

Tshishimbi ameanza mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ya jijini Kinshasa, baada ya kuachana na klabu ya Young Africans, kufuatia mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita.

Kiungo huyo alieonekana kuwa tegemeo wakati akiitumikia Young Africans, jana aliposti picha katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram akionekana pamoja na kocha wa AS Vita, Florent Ibenge.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu ukweli wa picha hiyo, alisema ni kweli na ameanza mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ambayo ina historia ya kupambana vilivyo kwenye michuano ya Bara la Afrika.

“Bado sijasaini mkataba na AS Vita ila mazungumzo yapo katika hatua nzuri tukiweza kukubaliana basi leo nitasaini mkataba tayari kwaajili ya kuitumikia msimu ujao,” amesema Tshishimbi.

Kiungo huyo mkabaji amesema maongezi yanaendelea vizuri na mambo yakikaa sawa atasaini kuwatumikia miamba hao.

Endapo AS Vita watafanikiwa kumtangaza Tshishimbi ni mchezaji wao mpya huenda akawa mbadala wa kiungo mkabaji, Mukoko Tonombe aliyeondoka klabuni hapo na kujiunga na Wananchi Young Africans.

Tshishimbi alijiunga na Young Africans mwaka 2017, akitokea Mbabane Swallows ya Eswatini zamani Swaziland na alidumu klabu hiyo ya jijini Dar es salaam kwa miaka mitatu mpaka mwaka huu, kufikia maamuzi ya kutokuongeza mkataba kwa sababu za kimaslahi ambazo zilielezwa.

Kwa kipindi chote cha miaka mitatu Tshishimbi aliyoitumikia Young Africans amefanya kazi na makocha tofauti waliopita hapo kama George Lwandamina, Mwinyi Zahera, Luc Eymael na Boniface Mkwasa.

Magufuli arusha jiwe gizani Singida, 'mwambieni nitampa kazi'
Menina : "Siwezi kutaja Dau langu"