Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imedhamini mashindano ya Soka la ufukweni kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Jijini Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika katika fukwe za Coco Beach Januari 07 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa Mkuu wa Mauzo kutoka Kampuni TTCL, Peter Ngota alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es salaam juu ya udhamini huo.

Amesema kuwa, mashindano hayo yanawalenga wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Jijini Dar es Salaam ambao ni wadau wakubwa wa Kampuni ya TTCL kupitia huduma ambazo wanazitoa kama vile vifurushi vya intanenti, dakika pamoja na ujumbe mfupi.

“Tumeamua kudhamini mashindano hayo kwa wanafunzi hao  kutokana na umuhimu wa michezo kwao katika kuwajengea amani, furaha na afya  njema ambavyo vitawawezesha kufanya vizuri katika masomo yao na hata kuwa wabunifu katika maeneo wanayosomea na kupelekea nchi kufikia uchumi wa kati,” amesema Ngota.

Vyuo vilivyothibitisha ushiriki wa mashindano hayo mpaka sasa ni Chuo cha Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT). Mashindano hayo hayatakuuwa na kiingilio na yataanza saa 3:00 asubuhi

Telegram yamkamatisha mtuhumiwa ugaidi Ujerumani
Kocha Salum Mayanga Arudishwa Taifa Stars