Meneja wa Klabu Bingwa chini Ujerumani Thomas Tuchel amesisitiza kuwa hana tatizo lolote la kibinafsi na Mshambuliaji wa klabu hiyo Thomas Muller, baada ya kuibuka kwa tetesi hizi kufuatia uamuzi wake wa kumuweka benchi katika michezo yote miwili ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya za Bayern Munich dhidi ya Manchester City.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 aliondolewa kwenye kikosi cha kwanza mjini Manchester na Munich, huku Bayern ikiondolewa kwa jumla ya mabao 4-1 na hivyo kutolewa katika hatua ya nane bora kwa msimu wa tatu mfululizo.
Muller ndiye mchezaji mwenye mafanikio zaidi katika historia ya Bayern, akishinda mataji 11 ya Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, na mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati wa maisha yake ya kifahari akiwa na Bavaria hao.
Ana nafasi ya kunyakua taji lingine la ligi ya nyumbani msimu huu, lakini hilo ndilo kombe pekee ambalo Bayern wamebakia kuliwania baada ya kuondoka Ulaya na kufungwa na Freiburg katika Robo Fainali ya kombe la Ujerumani, DFB-Pokal.
Ilidaiwa kwamba, Tuchel aliyeteuliwa hivi karibuni alitofautiana na gwiji wa klabu hiyo Muller, lakini kocha huyo amekanusha kama kuna tatizo lolote kati ya wawili hao.
“Mimi mwenyewe ni shabiki mkubwa wa Thomas Muller. Ana sifa ya kiwango cha juu duniani,” alisema Tuchel katika mkutano na waandishi wa habari juzi.”
“Mechi za Manchester hazijamfaa kikamilifu. Vinginevyo, pengine angecheza. Michezo mingi ni michezo ya Muller.”
“Kila kitu kiko sawa kwa sasa. Nilifurahishwa na majibu yake kwenye uwanja wa mazoezi juzi. Nilifurahishwa sana. Aliishughulikia kwa njia ya kupigiwa mfano.”
“Lakini lazima nifanye maamuzi yangu, wakati mwingine huwa magumu. Hakuna maelezo ya kibinafsi ndani yake.”
Kila mtu anapaswa kukubali katika hali ya ushindani.” Tuchel amewataka Bayern waonyeshe ubabe zaidi katika michezo yao iliyosalia, akisema timu hiyo imekosa “azma na kasi”.
“Ni muhimu jinsi timu inavyoshughu likia hali hiyo. Mengi yametokea msimu huu,” alisema Tuchel. “Timu ina uzoefu mwingi.”