Jamii nchini, imetakiwa kujengewa uwezo wa kutambua na kuweka mkazo kwenye upatikanaji wa tiba ya saikolojia na ushauri nasaha ili kuwasaidia waathirika wa matukio ya udhalilishaji kukabiliana na changamoto za kisaikolojia zinazowaathiri baada ya kufanyiwa vitendo hivyo.

Ushauri huo, umetolewa na wanasaikolojia Zanzibar wakati wa mafunzo kwa familia za waathirika wa matukio hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark – DANIDA, kuwajengea uwezo kwa lengo la kupunguza athari za kisaikolojia na kijamii.

Mwanasaikolojia, Hussein Mohamed akizungumza wakati wa mafunzo.

Wameeleza kuwa, ukosefu wa elimu kuhusu umuhumu wa tiba ya saikolojia na ushauri nasaha inapelekea waathirika wengi kuchukua maamuzi yanayoongeza zaidi vitendo vya ukatili kwenye jamii ikiwa ni pamoja kujichukulia hatua mkononi ikiwemo kujiua na wakati mwingine kuwaumiza wengine kimwili na kisaikolojia.

Aidha, walibainisha kwamba zipo njia mbalimbali za kutoa huduma ya saikolojia na ushauri nasaha ambazo ni muhimu kutolewa kwa waathirika ikiwa ni utoaji wa huduma kwa waathirika pamoja na familia zao ili kutambua namna ya kukabiliana na hali husika bila kuwaathiri zaidi.

 Asia Saleh, akizungumza wakati wa mafunzo kwa familia za waathirika wa matukio hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kuwajengea uwezo kukabiliana na hali baada ya kukukumbwa na vitendo hivyo kwa lengo la kupunguza athari za kisaikolojia na kijamii zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake Mwanasaikolojia, Hussein Mohamed ameeleza suala la tiba ya saikolojia na ushauri nasaha ni changamoto katika jamii kutokana na kukosekana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa tiba hiyo na kupelekea waathirika wengi kuumizwa zaidi kisaikolojia bila kupata msaada sitahiki.

Awali, Mwanasaikolojia Asia Saleh, aliwahimiza wazazi na walezi kuwa tayari kuwatafutia msaada wa kisaikolojia waathirika wa matukio hayo ili kuepusha madhara zaidi na kusema, “wazazi jitahidini kuwakutanisha mapema waathirika wa udhalilishaji na washauri nasaha ili wawasaidie kuwarejesha katika hali zao za kawaida na kuwaepusha na athari zaidi za kisaikolojia zinazoweza kuwakumba kutokana na kufanyiwa vitendo hivyo,”

TAMWA – ZNZ, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark – DANIDA, linatekeleza mradi wa kutumia jukwaa la habari kumaliza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar ambapo kupitia mradi huo waathirika wa matukio hayo wanajengewa uwezo wa kisaikolojia ili kuwa tayari kusimama kutoa ushahidi katika vyombo vya sheria na kupata haki zao.

Ndalichako atangaza mema ya Tanzania jijini Geneva
Tanzania yazindua rasmi ubalozi wake Vienna, Autsria