Aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema ni vyema kujenga mazoe ya kusoma vitabu ili kujiongezea maarifa huku akitumia msemo wa Mwandishi na mhamasishaji Rick Warren kuwa “the moment you stop learning, you stop leading.” akimaanisha ukiacha kusoma unaacha kuongoza.
Msigwa, ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano na Dar24 nyumbani kwake Kihesa mjini Iringa nakuongeza kuwa maarifa ya mtu huongezeka kwa kusoma vitabu mbalimbali vyenye ubora na maarifa vinavyoweza kumsaidia mtu kupiga hatua.
Amesema, “Kama kuna mtu amefanikiwa zaidi yako, kwenye eneo lolote la maisha, kuna vitu anajua ambavyo wewe hujui badala ya kumwonea wivu au kumwogopa, mwombe akushirikishe ni aina gani ya vitabu anasoma, hapo utapata vya kuanzia.”
Aidha, ameongeza kuwa uongozi unahitaji weledi na maarifa mapya na kwamba upo umuhimu wa kuihimiza jamii juu ya umuhimu wa kusoma vitabu kuanzia ngazi ya msingi, ikiwemo umakini wa uchaguzi wa vitabu ambavyo vinaweza kumpa mtu hamasa na kufikia malengo kusudiwa.
“Kwa bahati mbaya sana, kutafakari ni kitu unachopaswa kukifanya mwenyewe, kwa sababu ni wewe pekee unayeyajua maisha yako kwa undani watu wawili mnaweza kusoma kitabu kimoja na wote mkakielewa, lakini hatua za kuchukua zikawa tofauti, kwa sababu maisha yenu ni tofauti,” Amesema Msigwa.
Peter Simon Msigwa (57), ni mwanasiasa maarufu nchini na aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kwa vipindi viwili kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye kwasasa anaendelea na shughuli za kisiasa huku akijihusisha na Kilimo.