Mtuhumiwa mmoja wa uvamizi uliotekelezwa na genge la majambazi kwa mwanamke mmoja mtaani Rongai nchini Kenya, amekamatwa na maafisa wa polisi akitoa kiasi kikubwa cha pesa kwenye duka la kutolea pesa
Mwanamume huyo ambaye sasa anawasaidia polisi katika msako wa kuwakamata wenzake, alikamatwa Jumatatu mtaani Mwiki, Kasarani akitoa shilingi 240,000 za Kenya kutoka duka la Mpesa.
Mtuhumiwa huyo anaaminika kuwa mwanachama wa genge la wezi ambao walikuwa wamejihami kwa bunduki na kumwibia mwanamke huyo mkoba wake, simu na vitu vingine vya bei ghali pamoja na kumshurutisha kuwapa nambari yake ya siri (PIN) ya Mpesa.
Mhudumu wa duka la Mpesa ambako pesa hizo zilitolewa pia alikamatwa na maafisa wa polisi ili kusaidia katika uchunguzi.
“Kufikia sasa tumekamata washukiwa wawili. Tunaendelea kuwahoji ili kupata taarifa zaidi,” afisa huyo amenukuliwa akisema.
“Ripoti za awali zinaonyesha kuwa kikosi cha majambazi ambacho kilimvamia mwanamke huyo kiliongozwa na afisa wa polisi wa zamani,” alisema.
Waziri wa Usalama wa Kenya Fred Matiang’i alitembelea eneo la tukio akiwa ameambatana na Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai na Mkuu wa Kitengo cha Huduma Spesheli katika Idara ya Upepelezi wa Jinai (DCI) Pius Gitari na kuwahakikishia wakazi kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa.
Ziara ya watatu hao pia ilidhamiria kufahamu hali halisi ya usalama eneo hilo, kukiwa na malalamishi ya wakaazi ambao wamelalamika kudorora kwa usalama na kuhimiza polisi kuchukua hatua.