Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta amesema kuwa moja ya makosa ambayo yalipelekea timu ya taifa ya Tanzania kupoteza mchezo wake dhidi ya Kenya, ni wachezaji wa Tanzania kushindwa kulinda ushindi ambao waliupata kwenye kipindi cha kwanza.
Ameyasema hayo baada ya kumalizika kwa mchezo ambao Stars ilifungwa kwa taabu bao 3 -2 na kuifanya kushika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa kundi C lenye timu za Algeria, Senegal na Kenya.
“Mimi nafikiri ni timu nzima tulishindwa kulinda ushindi wetu, bado tupo kwenye mashindano naamini siku zote kuanguka ni kujifunza, sisi tupo na tunaendelea kupambana, kama Mungu yupo na sisi tunaendelea kumwamini, nadhani Watanzania tumewaangusha sana na tungeweza kuwa na matokeo chanya leo.” amesema Samatta
Aidha, katika mchezo wa jana mabao ya Taifa Stars yalifungwa na Simon Msuva dakika ya 6 huku bao la pili la Stars likifungwa na Mbwana Samatta akifunga dakika ya 40, ambapo mabao ya Kenya yamefungwa na Michael Olunga dakika 39, 82, na Omollo.
Hata hivyo, mechi ya mwisho ya Taifa Stars inacheza na Algeria Julai 1, 2019 ambapo nafasi pekee iliyobaki ni Taifa Stars kushinda mchezo huo, na watakuwa na nafasi kubwa ya kupita kwa nafasi ya upendeleo maarufu kama Best Looser endapo atafikisha alama 3, huku akitegemea mchezo wake dhidi ya Kenya na Senegal mmoja wapo ashinde na Taifa Stars ipate ushindi wa zaidi ya mabao matatu.