Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omari Juma Kipanga amesema serikali ipo kwenye mikakati ili kuhakikisha wanafunzi wanaopata ujauzito wanarudi kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua.
Ameyasema hayo katika kongamano la wadau na wachangiaji wa elimu lililoandaliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA na kufanyika katika Chuo Kikuu Cha Dar es salaam likiwa na lengo kujadili na kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha kuzitatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu nchini.
“Suala la kupata elimu ni haki kwa kila mtanzania hivyo utaratibu utawekwa ili kuhakikisha waliopata ujauzito wanarejea kuendelea na masomo,” Amesema Kipanga.
Aidha Naibu Kipanga amesema pamoja na jitihada za kukarabati na kujenga miundombinu mbalimbali bado serikali imeweka nguvu katika kuboresha vyuo vya ualimu ili viweze kuzalisha walimu watakoendana na kasi ya Teknolojia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bahati Geuzye amesema zaidi ya shilingi Bilioni 9.1 zilitumika kufadhili miradi 96 ya elimu katika shule 88 na taasisi moja ya sayansi na teknolojia kwa mwaka wa fedha 2019/2020, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shule 116 zinanufaika na miradiĀ 123 inayogharamia jumla ya shilingi Bilioni 9.4.
Akizungumza na Dar24Media Mkurugenzi huyo amesema kongamano hilo lenye kauli mbiu changia mfuko wa elimu boresha miundombinu ya elimu ni la muhimu kwa kuwakumbusha wadau mbalimbali kuendelea kuchangia mfuko wa elimu Tanzania.