Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini imekutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othman Chande, amesema tume imekutana na mabalozi hao kwa lengo la kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo wakiwa ni sehemu ya wadau.
Jaji Mkuu Mstaafu, Mohammed Othman Chande.
“Taasisi za Kimataifa wakati mwingine zinafanya kazi na taasisi za haki jinai, tumeona tuwafahamishe kwa kuwa nao ni wadau. Pia tunawakaribisha watoe mapendekezo yao kwa sababu huu sio mwisho wa kupokea maoni,” alisema Jaji Mkuu Mstaafu, Chande.
“Kwa sasa tunamalizia uchambuzi wa maoni yaliyokusanywa, kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kwa mwezi mmoja na baadaye itatolewa rasimu ya mapendekezo,” alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande na kuongeza kuwa rasimu ya mapendekezo itahusisha yanayopaswa kutekelezwa haraka, kwa muda wa kati na kwa muda mrefu.
Jaji Mkuu Mstaafu Chande alisema, “shauku kubwa ya wananchi ni kuona mageuzi katika taasisi za haki jinai na tunatarajia mapendekezo yetu yafanikishe hilo,” alisisitiza Jaji Mkuu Mstaafu Chande ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu takriban wananchi 10,000 wamesikilizwa, mikutano 25 ya hadhara, imefanyika katika Wilaya 53 na Mikoa 25 na tume imefanikiwa kuwasikiliza wadau mbalimbali.
Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab alisema tume hiyo iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuangalia njia bora ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.