Tume ya Madini nchini imetangaza zabuni kwa ya ununuzi wa maeneo 10 yenye leseni hodhi za madini na yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 ambayo leseni zake hizo zilirudishwa Serikalini.
Tangazo hilo limetolewa hii leo Desemba 19, 2019 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula katika mkutano na kamishna wa tume ya Madini Dkt. Athanas Macheyeki, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, watendaji wa tume ya hiyo na waandishi wa habari.
Amesema awali mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya sheria ya madini sura mamba 123 na kanuni zake ambapo pamoja na mambo mengine zilizokuwa leseni hodhi za madini zilirudishwa Serikalini.
“Baada ya marekebisho hayo maeneo yote 10 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yalirudishwa Serikalini na wachimbaji wa madini wengi wamekuwa wakiulizia maeneo hayo mara kwa mara lengo likiwa ni kuomba leseni za uchimbaji madini,” ameongeza Ptof. Kikula.
Aidha amebainisha kuwa baada ya uchambuzi kufanyika Serikali kupitia Tume ya Madini imeamua maeneo hayo yote 10 yaliyopo Ngara – Kagera, Kahama – Shinyanga, Chunya – Mbeya, Busega – Simiyu, Nachingwea – Lindi, Bariadi na Morogoro yatatolewa kwa zabuni.
Prof. Kikula ameongeza kuwa pia watakaribisha kampuni za uchimbaji wa madini na watu binafsi wenye uwezo wa fedha na utaalam katika miradi ya uchimbaji wa madini walio na nia ya kuendeleza miradi ya madini ya nickel, dhahabu na rare earth elements kuomba zabuni hizo.
“Sasa katika hatua hii mwekezaji yeyote atakayeonesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo tuliyoyaaimisha atakuwa na jukumu la kufanya kazi ikowepo na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wadodo wa madini,” amefafanua Prof. Kikula.
Akiongea katika kikao hicho Katibu mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya amewataka wamiliki na waombaji wote wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini wenye mapungufu kurekebisha matatizo waliyonayo ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya leo Desemba 19, 2019.
Prof. Manya pia ameelezea mapungufu hayo kuwa ni pamoja na leseni ambazo hazifanyiwi kazi, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka, maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi na maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria.
“Mapungufu mengine ni pamoja na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa hivyo ndani ya siku 30 kuanzia sasa wanatakiwa kuwa wameshaharekebisha mapungufu yao,” amesisitiza Prof. Manya.
Hata hivyo amesema mpaka sasa leseni zaidi ya 134 za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini hazijachukuliwa na zaidi ya maombi 450 ya leseni za utafutaji yana mapungufu na kudai kuwa kampuni au watu binafsi waliopewa leseni lakini wameshindwa kutekeleza masharti husika watafutiwa leseni kwa mujibu wa sheria ya madini.
Amesema pia leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango kwa mwaka, leseni ambazo hazifanyiwi kazi na leseni ambazo zimekwishatolewa lakini hazijachukuliwa zitaandikiwa hati ya makosa na yasiporekebishwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria.
“Na maombi yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa kati yenye mapungufu yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa pamoja na wachimbaji wadogo waweze kuomba maeneo hayo,” amefafanua Prof. Manya.
Hata hivyo amebainisha kuwa maombi ambayo yamekidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hayajalipiwa ada ya kuandalia leseni nayo yataondolewa kwenye mfumo ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuyaomba na kuyafanyia kazi.