Tume ya Mipango imeanza zoezi la kuwajengea uwezo wataalamu katika kuandaa na kutekeleza miradi ya maendeleo inayotumia fedha za serikali au kwa kushirikiana na Sekta binafsi kwa lengo la kuongeza nidhamu na weledi katika matumizi ya rasilimali za Umma.

 

Mafunzo hayo yanayoendelea katika moja ya kumbi za ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es salaam na kuendeshwa na wataalamu elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yanalenga kuanda wataalamu ambao watakwenda kutoa mafunzo kwa maofisa  wa Serikali walio chini ya idara za Sera na Mipango na zile za uwekezaji katika Wizara, Mikoa, Halmashauri, pamoja na mashirika na taasisi mbalimbali za umma hapa nchini.

 

Akifungua mafunzo hayo mwanzoni mwa Juma, Kaimu Katibu Mtendani kutoka Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuleta ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

“Shabaha kuu ya mafunzo haya ni kutoa maelekezo ya mchakato na hatua zinazohitajika kufuatwa katika kutayarisha na kutekeleza miradi yote inayotumia fedha za umma au kwa kushirikiana na sekta binafsi,” Alisema Bibi Mwanri.

 

Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa kutokana na kukithiri kwa  kasoro katika miradi ya maendeleo inayotumia fedha za umma, Serikali kupitia Tume ya Mipango ililazimika kuandaaMwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma (Public Investment Management Operational Manual) ambao utatumika katika kuandaa, kutekeleza na kusimamia miradi yote inayotumia fedha za umma au kwa kushirikiana na sekta binafsi.

 

Bibi Mwanri alieleza kuwa katika awamu hii ambayo Serikali imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda miradi mingi ya maendeleo inatarajiwa kuanzishwa. Hivyo, bila kuwa na uelewa wa pamoja moingoni mwa wadau wanaohusika katika kuandaa, kutekeleza na kusimamia miradi hiyo malengo ya  Mpango wa Pili wa Maendeleo hayatafikiwa kama inavyotarajiwa.

 

“Katika kipindi hiki ambapo bajeti ya maendeleo imeongezeka na kufikia asilimia arobaini ni wazi kuwa miradi mingi ya maendeleo inaanzishwa, hivyo ni lazima kila mtaalamu aelewe kuwa tunawajibu wa kuandaa miradi bora, yenye tija kwa wananchi na inayoendanda na thamani ya fedha zinazotumika,” Alisisitiza Bibi Mwanri.

 

Bibi Mwanri aliwataka wajumbe wote kuhakikisha wanatumia mafunzo hayo vizuri ili kupata uelewa wa kutosha juu ya mwongozo huo.

 

Mafunzo hayo ya siku tano yamehudhuriwa na  wajumbe kutoka Wizara, Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Asasi za Kiraia pamoja na Sekta binafsi na yanatarajiwa kuandaa wataalamu bora watakaokwenda  katika kanda mbalimbali nchini kutoa mafunzo tarajiwa kwa walengwa.

Waziri Wa Elimu Prof.Ndalichako Atoa Siku Saba Kwa Vyuo Vikuu Kurejesha Fedha Za Wanafunzi Hewa
Waziri Wa Afya Ummy Mwalimu Akutana Na Balozi Wa Israel