Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuchunguza taarifa zilizodai kuwa vyombo vya usalama vimewaamrisha wafanyakazi wake kukabidhi vitambulisho vya wapiga kura vilivyotolewa kwa mfumo wa BVR mwaka huu. Polisi na jeshi pia ni sehemu ya vyombo vya usalama vilivyotajwa kwenye taarifa hizo zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva amesema kuwa tume hiyo inafuatilia kwa ukaribu suala hilo na kwamba wamenzisha uchunguzi kubaini kama kuna ukweli wowote ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Sina taarifa rasmi kuhusu suala hilo, lakini nimesikia kwenye vyombo vya habari na nalifuatilia kwa ukaribu kwa kuwa jambo hili halikubaliki,” alisema mwenyekiti huyo wa NEC.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Malimu, alieleza kuwa chama hicho kimeanza kulifuatilia kwa karibu suala hilo pia ili kubaini kama kuna ukweli wowote kwa kuwa zoezi hilo limelenga hasa katika kuhujumu uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Taarifa hizo zinazosambaa mtandaoni zilidai kuwa makao makuu ya jeshi la polisi mkoa wa Pwani ni moja kati ya sehemu ambazo askari wameombwa kuwasilisha vitambulisho vyao. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Jaffary Mohammed alikanusha vikali taarifa hizo na kudai kuwa ni za uongo zilizotengenezwa kisiasa.

“Hizo ni taarifa za kisiasa tu. Hatujawahi kutoa tamko kama hilo, na kama jeshi la polisi hatutajihusisha na masuala ya kisiasa kamwe,” alisema Kamanda Mohammed na kuongeza kuwa kadi ya mpiga kura ni mali ya mpiga kura, hivyo hakuna namna yoyote ambayo polisi wanaweza kutoa amri kama hiyo.

 

City Hawaambiwi Hawasikii Kwa De Bruyne
CCM Yapasuka Arusha