Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na Kata 6 za Tanzania bara.
Tayari Tume imekwisha kupokea Barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuwa kiti hicho kiko wazi.
Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari Jijini Dodoma leo, 3 Juni, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Willson Mahera imesema uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 18 Julai,2021.
“Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ameitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha Ubunge katika Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,” alisema Dkt Mahera.
Kiti cha Mbunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kiko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Khatib Said Haji na hivyo kukoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Aidha, Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara.
“Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume imeandaa chaguzi ndogo ili kujaza nafasi ya Mbunge iliyo wazi katika Jimbo la Konde na nafasi za udiwani kwenye Kata sita (06) za Tanzania Bara,” alisema taarifa hiyo ya Dkt. Mahera.
Kata zitakazohusika katika uchaguzi huo ni Kata ya Mbagala Kuu Jimbo la Mbagala Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kata ya Diringish iliyopo jimbo la Kiteto, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Kata ya Mitesa, Jimbo la Lulindi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Kata nyingine ni Kata ya Gare, jimbo la Lushoto Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kata ya Mchemo,Jimbo la Newala Vijijini, Wilaya ya Newala mkoani Mtwara na Kata ya Chona, Jimbo la Ushetu, Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa wagombea inaanza Juni 21 hadi 27,2021 huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo ukifanyika Juni 27 mwaka huu.
Aidha, Dkt. Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika jimbo la Konde na Kata zitaanza Juni 28, 2021 na zitafikia ukomo wake Julai 17 mwaka huu na uchaguzi kufanyika 18 Julai,2021.
Mahera amesema tayari Tume imevitaarifu Vyama vya Siasa kwa njia ya barua juu ya kuwepo kwa uchaguzi huo mdogo na inavikumbusha kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, miongozo na maelekezo ya Tume wakati wote wa kipindi cha Uchaguzi.