Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa lengo la kuwasaidia wakulima wapate mitaji ili waongeze tija.
Pia amewataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wahahakikishe wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha miwa.
Waziri Mkuu amesema hayo wakati alipotembelea shama la miwa Mkulazi na MbIgiri mkoani Morogoro alipokuwa njiani kwenda jijini Dodoma.
Amesema lengo la kuanzishwa shamba la mwa la Mkulazi ni katika jitihada za Serikali za kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikikia katika kiwango kinachohitajika.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee ni kuboresha kilimo cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.
Amesema shamba hilo linaendeshwa kwa ubia kati ya NSSF na Jeshi la Magereza, hivyo, aliiagiza Menejimenti mpya ya Mkulazi kuhakikisha shamba hilo linasimamiwa kikamilifu.
Waziri Mkuu pia, alimuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike apeleke wataalamu wengi wa kilimo katika shamba hilo ili wasaidie kusimamia kitaalamu.
“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu, uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na watu binafsi,” alisema.
Kuhusu suala la maji hususan kipindi cha mvua ambayo huaribu shamba, Waziri Mkuu aliwataka watafute namna nzuri ya kuyahifadhi ili wayatumie kipindi cha kiangazi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watafute mashine nyingine zitakazotosha kumwagilia shamba hilo wakati wa kiangazi ili miwa isiharibike na iendelee kuwa ya kijani wakati wote.
Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenistar Mhagama, alisema shamba la Mkulazi II ni miongoni mwa mashamba mawili yanayomiilikiwa na wabia wawili yaani NSSF na Jeshi la Magereza.
Amesema walikubaliana wao na Magereza wafanye kazi kwa kuongozwa na uzalendo, maadili ya utendaji wa kazi, uaminifu ili mwisho wa siku mradi huo uwe na tija na uweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa.
Amesema wanaamini fedha zilizowekezwa kwenye mradi huo ambazo ni za wanachama zinatakiwa zirudishe faida kwa wanachama wenyewe na kujenga uchumi wa Taifa.
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha tatizo la upatikanaji wa sukari nchini linakuwa historia.
Amesema mbali ya shamba hilo la Mkulazi II pia kuna lingine la Mkulazi I ambalo ni kubwa zaidi, hivyo alishauri liendelezwe ili limalize tatizo la sukari nchini. Waziri Mkuu alimtaka ashughulikie shamba hilo kwa kuwa lipo Wizara ya Kilimo.