Waziri wa Utalii, Mohammed Mchengerwa, Naibu wake, Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu, Benedict Wakulyamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava aliongoza baadhi ya wajumbe wa Kamati hizo kushuhudia tukio hilo la kihistoria la makundi ya wanyama aina ya Nyumbu waliokuwa wakivuka Mto Mara.
Tukio hilo, limefanyika eneo la Kogatende lililopo Serengeti, ambapo wageni mbalimbali kutoka mataifa mengi waliungana na viongozi hao wakishuhudia kwa zaidi ya saa 2 wanyama hao waliokuwa wakisindikizwa na pundamilia wakivuka na kupitia majaribu mbalimbali, ikiwemo kukabiliana na mamba kwenye Mto huo.
Akizungumza eneo hilo, Mchengerwa amesema “ndio tumeanza kutekeleza mikakati kabambe ya kuutangaza utalii wetu,tukio hili ni la kihistoria na huwezi kulikuta popote Duniani ujio wetu hapa ni kulipa tukio hili heshima na kulitangaza zaidi duniani.”
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava akiongea mara baada ya tukio hilo alisema, “tumejionea maajabu na tunaipongeza Serikali na wahifadhi wetu kwa kuwalinda wanyama hawa mpaka leo tumejionea tukio hili la aina yake.”