Afarah Suleiman – Manyara.
Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga amewataka Madereva wa Bodaboda, Babaji, Baba na Mama lishe kutumia fursa ya ya kibiashara kwa kuwahudumia wageni watakaofika kwenye sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru ili kujitengenezea kipato.
Sendiga ametoa wito huo hii leo September 20, 2023 wakati akizungumza na makundi hayo mjini Babati, zoezi lililoendana na utoaji wa vizibao na stika kwa Madereva zenye ujumbe wa Mwenge kuhusu utunzaji wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kilele cha mbio hizo Oktaba 14, 2023 zitakazofanyika uwanja wa michezo wa Kwaraa mjini Babati.
Amesema wote kwa pamoja mbali na maandalizi ya kilele hicho cha Mwenge pia wanatakiwa kuzingatia Sheria za usalama Barabarani, ikiwemo kusimama kwenye taa nyekundi na alama zingine muhimu ili kuepusha ajali zisizo za lazima zinazopelekea wengi wao kupoteza maisha au kupata vilema vya kudumu.
Kuhusu Baba na Mama Lishe, Sendiga amewataka kuzingatia usafi wa Miili, Chakula, mazingira ya kupikia na ya kuuzia Vyakula ikiwemo kuwa waaminifu na wakarimu kwa kila aina ya huduma watakazotoa kwa wageni kwani baadhi yao wameanza kuingia hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi ili kuhakikisha Mkoa na wageni wanakuwa salama.
Kilele cha mbio za Mwenge wa uhuru mwaka huu itaambatana na kilele cha wiki ya Vijana kitaifa itakayozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Oktoba 10, 2023 pamoja na kumbukumbu miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.