Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania walioshiriki katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia wahakikishe wanatumia vizuri fursa walizozipata kutoka kwenye jukwaa hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wafanyabiashara walioonesha nia ya kuja kuwekeza nchini.
Majaliwa ameyasema hayo katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa lengo la kuwatambua wafadhili na washiriki wa Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia.
Amesema, Serikali imeondoa tozo na urasimu uliokuwepo awali kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara na uwekezaji nchini na kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanatakiwa kuhakikisha Taifa linanufaika kwa kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya uwekezaji na kuwashawishi wawekezaji kutoka nchi wanazoishi waje kuwekeza Tanzania.
Waziri Mkuu ambaye yuko Italia akimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Rome nchini Italia, aliwasisitiza Watanzania waheshimu sheria za nchi husika.
Kupitia jukwaa hilo wafanyabiashara na wawekezaji wengi kutoka nchini Italia wameonesha nia ya kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa wizara zinazohusika na masuala ya uwekezaji kuchangamkia fursa hiyo.