Mbunge wa Singida Mashariki ambaye ni mwanasheria Mkuu wa Chadema, jana alitumia saa mbili Mahakamani kupangua hoja zilizowasilishwa mahakamani na wapiga kura wanne wanaopinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mbunge wa Bunda Mjini Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wasira (CCM).

Wapiga kura hao wanne ambao wametajwa kwa majina ya Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malegele walifungua kesi hiyo wakidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki na kwamba ulitawaliwa na vitendo vya rushwa na udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuzidi kwa vituo vya kupigia kura. Wananchi hao wanaitaka Mahakama kutengua ushindi wa Bulaya wakimtetea Wassira.

Akijibu hoja hizo kwa saa mbili mfululizo (saa 4:10 asubuhi – saa 6 mchana) mbele ya Jaji Lameck Mlacha, Lissu aliitaka mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya walalamikaji akidai kuwa katika maombi yao wameshindwa kutoa hoja mahususi zinazoonesha ukiukwaji wa sheria na taratibu uliotajwa.

Alieleza kuwa waleta maombi wameeleza kuwa kuna vitendo vya rushwa lakini wameshindwa kueleza wazi mhusika wa vitendo hivyo vya rushwa pamoja na kuainisha athari walizozipata kama wapiga kura.

“Lakini madai ya juujuu tena ya jumla kuwa aliyetoa rushwa ni wakala wa mteja wangu, hayakubaliki mbele ya macho ya sheria kwa sababu mtu huyo hajulikani na ni jukumu la mleta maombi kuthibitisha madai, uthibitisho huo hauko kwenye hati ya maombi yao,” Lissu aliiambia Mahakama.

Mahakama ilitoa nafasi ya kupumzika na kurejea baada ya saa mbili ili kutoa nafasi kwa upande wa walalamikaji kujibu hoja hizo.

 

TCRA kuwashughulikia wanaotumia majina ‘feki’ mitandaoni
Orijino Komedi wakamatwa, wakutwa na vifaa vya Jeshi la Polisi