Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amesema kuwa changamoto ya upinzani katika Bunge la Kumi na Moja imepelekea baadhi ya watu kuliona kama Bunge hatari kwao.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki amesema kuwa kutokana na kuwa na mtazamo huo, baadhi ya watu wenye maslahi binafsi wamefanya mchakato wa kulidhoofisha.

“Kuna watu ambao wanaamini kwamba hili Bunge limekuwa ni hatari inabidi lidhibitiwe. Na Bunge limekuwa hatari kwa sababu gani… hili Bunge limeibua mambo makubwa ambayo yameifanya serikali ifanye maamuzi ambayo haikuyataka,” Lissu alieleza kwenye mahojiano maalum na Azam TV.

“[Wanaamini] Bunge limekuwa hatari, limeweza kuibua uchafu serikalini, limeangusha mawaziri, kwahiyo inabidi lidhibitiwe. Sasa namna ya kulidhibiti, vuruga kamati zake kama nilivyoeleza. Pili, liondoe hewani,” aliongeza.

Lissu alieleza kuwa sababu zinazowaogopesha watu hao ni kwamba Bunge limekuwa likipendwa sana na wananchi kwa sababu wakati kukiwa na vikao vya Bunge wananchi wengi wamekuwa wanafuatilia kwa ukaribu kwa sababu wanajua Bunge lina athari (consequence).

Alipoulizwa kama wapinzani wataendelea kutumia mfumo wa kutoka nje ya vikao vya Bunge kila wanapopinga mwenendo na maelekezo wanayodhani hayako sahihi na namna gani wataweza kuiondoa hiyo aliyoiita ‘viongozi wa serikali kuona Bunge ni hatari’, alieleza;

“Tutapambana, Watanzania wasiwe na shaka sisi tutapambana. Tutapambana ndani ya Bunge, tutapambana nje ya Bunge. Ndani ya Bunge ikiwezekana… na nje ya Bunge kama ndani ya Bunge haiwezekani.”

Jenerali Mwamunyange Aimudu 'Hapa Kazi Tu' ya Magufuli, aongezwa Muda
Bomoabomoa yaikumba 'Coco Beach', yaja kivingine

Comments

comments