Tunisia imezuia ndege za Umoja wa Falme za Kiarabu za ‘Emirates’ kutua katika ardhi yake baada ya wanawake wa nchi hiyo kuzuiwa kupanda ndege hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo kulaani vikali vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi wa rangi vinavyofanyika dhidi ya wanawake wa nchi hiyo na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya ndege za Emirates.

Akizungumzia hatua hiyo, waziri wa usafiri wa Tunisia amesema kuwa uamuzi huo utaendelea kusimamiwa hadi pale Emirates watakapoendesha shughuli zao za usafiri wa anga kwa kuzingatia sheria na kanuni za Kimataifa.

Naye waziri wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Anwar Gargash amesema kuwa kulikuwa na kuchelewa katika kufanya mawasiliano ya kiusalama na Tunisia.

“Tunawathamini sana wanawake wa Tunisia na tunawaheshimu,” Waziri Gargash aliandika kupitia Twitter.

“Tumewasiliana na ndugu zetu wa Tunisia kuhusu taarifa za kiusalama ambazo ni muhimu na mchakato wake ulikuwa unaendelea,” aliongeza.

Maafisa wa Tunisia walieleza kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu ulizuia wanawake wa nchi hiyo kukanyaga katika ardhi yake na kwamba wamemtaka Balozi wa Falme hizo kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu uamuzi huo.

Tunisia imekuwa ikijaribu kurejesha na kuimarisha uhusiano wake na Umoja wa Falme za Kiarabu ambao ulivunjika wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011.

Rais Mpya wa Zimbabwe azidi kuwavuta wanajeshi
Dkt. Shein awatahadharisha wanaodhani ni mpole