Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amewaonya askari wake kuwa wasiwe kikwazo kwa wafanyabiashara nchini ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakuwa waadilifu kwenye suala la ulipaji wa kodi.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam, wakati akizungumza na Maofisa na Wakaguzi wa jeshi hilo ambapo amesema kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa askari anayeshiriki kwenye matukio yatakayoikwamisha nchi.
Amesema kuwa lengo kubwa ni kufanya tathmini kwa miaka 2 iliyopita kuwa wamefanya nini na kipi ambacho hawajafanya, pia amesisitiza kuwa wao wasiwe vikwazo kwa wafanyabiashara kwa sababu mishahara yote wanayolipwa inatokana na kodi za wafanyabiashara.
Aidha, ameongeza kuwa suala la weledi ni muhimu sana kwa hiyo amewataka kujua mbinu za kivita hivyo ni lazima kujua kupeleleza na mapambano ya silaha.
“Suala la weledi ni muhimu sana lazima ujue mbinu za medani za kivita, lazima ujue kupeleleza na mapambanao ya silaha ni lazima tulipeleke jeshi vizuri, kwa sababu tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa tunahakikisha unaenda vizuri, pia kwa uchaguzi wa 2020 lazima tuanze maandalizi leo,” amesema IGP Sirro.