Serikali ya Jamhuri ya Malawi imekabidhi tuzo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua mchango wake wakati wa maafa ya Kimbunga Freddy kilichotokea Machi, 2023 nchini humo.
Tuzo hiyo, imekabidhiwa na Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Jeshi la Ulinzi la Malawi, Brigedia Jen. Luke Mwetseni alipotembelea nchini akiwa na wanafunzi na wakufunzi kutoka Chuo hicho wakilenga kubadilishana uzoefu na kujifunza namna Tanzania inavyosimamia masuala ya menejimenti ya maafa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Malawi kwa kutambua mchango uliotolewa wakati nchi hiyo ilipopata maafa yaliyosababishwa na Kimbunga hicho, huku akisema Tanzania itaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo.
Alisema, “tumeipokea tuzo hii kwa heshima na tunatoa shukrani nyingi kwa namna mlivyojali na tunaahidi kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kati yetu na Malawi pamoja na Nchi nyingine.Kipekee tunampongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha diplomasia na mataifa mengine.”