Mwekezaji katika klabu ya Simba, Mohammed Dewji ameanzisha tuzo maalum ambazo amezipa jina la Mo Simba Awards na zitakuwa zikitolewa kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa klabu hiyo.
Tuzo hizo zitakazofanyika kwa mara ya kwanza tarehe 11 mwezi Juni katika Hoteli ya Hyatt Regency zinalenga kutambua mchango wa wachezaji, viongozi na mashabi ambao juhudi zao zimeiwezesha Simba SC kupata mafanikio iliyonayo sasa.
Utolewaji wa tuzo hizo utaleta changamoto kwa wachezaji kujituma zaidi kwani washindi wa tuzo zitakazotolewa katika vipengele mbalimbali watakuwa na deni kuhakikisha msimu ujao wanaendelea kufanya vizuri ili wabaki kwenye tuzo.
Kwa wachezaji ambao hawatapata tuzo ni wazi kwamba wataongeza bidii ili kufanya vizuri kuweza kushinda tuzo wakati mwingine jambo ambalo litaleta faida kwa klabu.
Vilabu kama Manchester United barani Ulaya vimekuwa na utamaduni wa kutoa tuzo mwishoni mwa msimu kwa wachezaji mbalimbali waliofanya vizuri hivyo mpango huu aliokuja nao Mo Dewji utakuwa na tija kwa klabu ya Simba.